Serikali ya Tanzania imepiga marufuku vituo vya Umma kuwalipisha wananchi wanaokwenda kupima maambukizi ya ugonjwa wa Malaria kwa kipimo cha MRDT na utoaji wa dawa za mseto (ALUU) zinazotumika kutibu ugonjwa huo kuanzia sasa.
Akizungumza na waandishi wa habari wakati wa kilele cha maadhimisho ya siku ya Malaria duniani mjini Dodoma, Waziri wa Afya, Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wazee na Watoto Bi. Ummy Mwalimu amesema vipimo hivyo ni bure na pia mgonjwa asilipishwe fedha kwa dawa za mseto.
“Napenda kusisitiza vituo vya umma vinavyotumia vipimo vya MRDT kwa wagonjwa wa malaria, vipimo hivyo ni bure na pia mgonjwa asilipishwe fedha kwa dawa za mseto ama yule anayelazwa kuchomwa sindano ya ugonjwa huo….Waganga wakuu wa mikoa na wilaya, hakikisheni kuanzia sasa mnafuatilia wahudumu wote na watakaokiuka agizo hili watachukuliwa hatua za kisheria mara moja”. Alisema Bi. Ummy
Aidha, Bi. Ummy amewataka wananchi kushirikiana na serikali kuwafichua wahudumu wa Afya ambao watawalipisha fedha pindi watakapo kuwa wanapima huduma ya Malaria kupitia kipimo cha MRDT ama watakapohitajika kupewa dawa ya mseto (ALUU), pia amezionya maabara binafsi ambazo zimekuwa zikifanya kazi zake kwa kuangalia zaidi fedha badala ya maisha ya mtu kama kuwaambia wana maambukizi ya malaria wakati hawana.
EmoticonEmoticon